Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeidhinisha azimio linalozitaka
nchi kuchukua hatua ya kuzuia usajili na usafirishaji wa wapiganaji wa
kigeni nchini Iraq na Syria.
Azimio hilo lililoidhinishwa kwa kauli moja na baraza hilo lenye nchi
wanachama 15 linayahitaji mataifa yote kuidhinisha sheria ambazo
zitafanya iwe ni uhalifu kwa raia wake kujiunga na makundi yenye itikadi
kali kama vile Dola la Kiislamu – IS na Al-Nusra Front. Rais Barack
Obama wa Marekani aliyeongoza kikao hicho maalum, amezitaja hatua hizo
kuwa ni za "kihistoria", ikiwa ni mara ya sita pekee katika historia ya
Umoja wa Mataifa ambapo Baraza hilo limewahi kukutana katika kiwango cha
viongozi wakuu wa nchi:Hata hivyo, Obama alionya kuwa "maazimio hayo pekee hayatoshi" na akatoa wito kwa serikali kushirikiana katika kuzuia usafirishaji wa wapiganaji wa kigeni nchini Iraq na Syria "siyo kwa siku chache zijazo, bali kwa miaka mingi ijayo".
Azimio hilo lililotayarishwa na Marekani linazitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya raia wanaosafiri au wanaopanga kusafiri kwenda nchi nyingine ili kujiunga na makundi ya itikadi kali na pia linapiga marufuku ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya usajili wa wapiganaji.
Takribani wapiganaji wa kigeni 15,000 kutoka nchi 80 wamejiunga na wapiganaji wa siasa kali nchini Syria, kwa mujibu wa takwimu za kijasusi za Marekani. Wataalamu wanasema kuwa idadi kubwa ya wapiganaji wa kigeni walioko sasa nchini Syria na Iraq wanatokea Mashariki ya Kati na nchi za Kiarabu, huku Saudi Arabia, Tunisia na Morocco zikiongoza kwenye orodha hiyo.
Mateka wa Kifaransa achinjwa Algeria
Azimio hili la Baraza la Usalama limesadifiana kupitishwa siku ile ile ambapo wanamgambo wenye itikadi kali nchini Algeria wametoa vidio inayoonesha wakimchinja mateka wa Kifaransa aiyekamatwa Jumapili iliyopita, Herve Gourdel ili kuiadhibu Ufaransa kwa kujiunga katika mashambulizi ya anga dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, nchini Iraq.
Akionyesha kuunga mkono azimio hilo dhidi ya ugaidi, Rais Francois Hollande wa Ufaransa alisema kuwa tukio hilo ni ishara kuwa ugaidi unastahili kukabiliwa kwa dharura na akatoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuungana katika vita hivyo. Hollande alisema tukio hilo la kinyama haliwezi kuzuia azimio la kuuangamiza ugaidi, na kuwa Ufaransa itaendeleza mashambulizi yake kwa muda usiojulikana.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP