Aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Nchini (TBS), Charles Ekelege amehukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwenda jela miaka mitatu na kuilipa serikali Dola 42,543 za Kimarekani, baada ya kupatikana na hatia ya makosa matatu ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka kwa kutoa asilimia 50.
Kadhalika, Ekelege anadaiwa kutoa asilimi hiyo ya punguzo la tozo ya utawala kwa Kampuni mbili Kampuni ya Jaffar Mohamed Ali Garage na Kampuni Quality Motors na kulisababishia shirika hilo hasara ya dola hizo.
Hukumu hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi Augustina Mmbando baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili na mahakama yake kumuona mshtakiwa bila kuacha shaka ana hatia.
Hakimu alisema ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri ulieleza mahakama kwamba mshtakiwa kupitia wadhifa wake alifanya maamuzi bila kinyume na sheria za TBS zinazomwelekeza kuwasilisha masuala yote ya kiutendaji kwenye Bodi ya Wakurugenzi.
Alisema kitendo cha kutoa msamaha kwa kampuni hizo bila kuacha shaka moja kwa moja mahakama imeona alitumia madaraka yake vibaya.
“Kwa upande wa shitaka la pili, kiongozi yeyote katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anapokuwa madarakani ni kwa ajili ya maslahi ya taifa, lakini mshtakiwa alikosa uzalendo na kutumia madaraka yake vibaya kuhujumu uchumi” alifafanua hakimu kuhusu ushahidi wa Jamhuri.
“Mahakama inamuona mshtakiwa ana hatia katika kosa hili la pili la kujumu uchumi … pia mshtakiwa amesababisha watanzania waliompa dhamana kukosa kula keki ya taifa lao kwa kujinufaisha yeye binafsi” alisema hakimu huyo na kuongeza kuwa.
“Katika ushahidi uliotolewa na mshtakiwa alikiri kufanya maamuzi bila kupata baraka na kibali cha Bodi ya Wakurugenzi na kwamba aliidanyanya mahakama” alisema Hakimu Mmbando.