MRATIBU wa Chama cha watu wenye maambukizi ya VVU kwa
watumishi wa Serikali Wilayani Chunya, Revocatus Rugeiyamu hivi karibuni
ametuhumiwa kufuja fedha za Ruzuku za chama hicho.
Kwa mujibu wa wajumbe hao, waraka uliotolewa na Serikali
unabainisha kuwa watumishi wa umma wanapaswa kusaidiwa na serikali kwa
kuwapatia huduma kama vile usafiri wa kwenda kwenye vituo vya ushauri nasaha na
posho za kujikimu.
Walisema kuwa waraka huo ulianza kutumika Novemba mosi mwaka
2006 lakini jambo la kushangaza ruzuku hizo zimekoma tangu zilipotolewa mwaka
2011 ambapo kila mlengwa alipatiwa kiasi cha Sh. 150,000 licha ya kuwa Mratibu
alikusanya kadi za mahudhurio kliniki kwa waathirika na kuziombea fedha za
kuwalipa kila mwezi.
"Mratibu wetu alikusanya kadi zetu kwa lengo la kwenda kuombea fedha kwenye mfuko wa ruzuku, lakini tangu tulipopatiwa mwaka 2011 hadi sasa hatujapatiwa tena wakati ni kila mwezi tunapaswa kulipwa," Alisema mmoja wa wajumbe hao.
Hali hiyo imewafanya waandike barua ya malalamiko yao kwa
menejimenti ya utumishi wa Umma yenye namba za kumbukumbu C/AC56/221/01/C/62
ikimtuhumu Mratibu huyo kufuja fedha zao na kuwanyanyapaa kila wanapohoji ni
kwa nini hawapatiwi.
Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya Esther Mwakalila alishindwa kulielezea
suala hilo ofisini kwake kwa maelezo kwamba mwenye maelezo ya kina ni afisa
utumishi wa wilaya hiyo Solomon Kimilike.
Kimilike alikiri kutengwa Shilingi Milioni 15 katika
kipindi cha mwaka 2013 na 2014 ambazo ameahidi kuwa mwishoni mwa mwezi Juni
walengwa watapatiwa huku akifafanua kwamba tatizo lilikuwa ni wao kutojitokeza
ili kuorodhesha majina yao.
Alisema ni watumishi 9 pekee waliojiorodhesha mbali ya
jitihada za halmashauri kutoa elimu kuhusu mapambano ya maambukizi ya VVU
pamoja na fungu hilo la kujikimu.
Hata hivyo maelezo ya afisa huyo yanakinzana na maelezo ya
walalamikaji ambao walisema walijiorodhesha na kadi zao kukusanywa hadi kufikia
idadi ya watu 80 na kufanikiwa kulipwa Sh. 150,000 kila mmoja.
