UNUNUZI HOLELE WA TUMBAKO WAOMBWA KUDHIBITIWA


SERIKALI imeombwa kudhibiti ununuaji holela wa tumbaku unaofanywa na wafanyabiashara wasio na vibali (walanguzi) toka nje ya nchi na kulikosesha taifa mapato.

Ombi hilo limetolewa ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya kuzinduliwa kwa msimu wa mauzo ya zao hilo, ambapo inadaiwa kuwa, katika msimu uliopita wa 2012/13 jumla ya tani 30 zilitoroshwa na walanguzi hao , ambao baadhi yao ni kutoka nchini Malawi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Meneja wa chama  kikuu cha ushirika cha wakulima wa tumbaku nchini (CHUTCU ltd), Wilaya ya Chunya,Bakari Kasia, alisema serikali inapaswa kuwa makini na kuwadhibiti walanguzi hao.

Alisema uzinduzi rasmi wa ununuaji wa zao hilo la tumbaku unatarajia kufanyika Mei mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro ndiye an atarajia kuwa mgeni rasmi.

Alisema kuwa kitendo hicho wafanyabiasha wa nje ya nchi kuingia na kutoroshea nje tumbaku ni changamoto kubwa kwa chama hicho kushindwa kufikia malengo yake ya kukusanya na kulipa ushuru na kodi za serikali.

“Kwani katika msimu wa 2011/ 12, chama kilishindwa kufikia malengo yake ya kukusanya kiasi cha kilogramu 12,800,000 na badala yake tuliambulia kilogramu 11,165,049.” Alisema.

Kwa mujibu wa Kassia, wafanyabiashara hao wa Malawi hufanikiwa kupata tumbaku nyingi kutokana kwa wakulima kutokana na wao kulipa fedha taslimu, tofauti na ilivyo kwa vyama vya ushirika ambavyo hutoa malipo hayo kwa awamu mbili katika msimu mmoja wa kilimo.

Hata hivyo alisema kwa kutumia udhaifu huo wa wakulima kutaka kulipwa kwa fedha taslimu, wafanyabiashara hao wamekmua wakiishia kuwalangua wakulima kwa bei ndogo ya shilingi  3500 bila kujali upangaji wa madaraja ya zao hilo ili kupata ubora wake.

 “Mbali na hawa jamaa kulipa keshi, lakini pia wao wamekuwa wakilipa bei ya juu kidogo, kwani kwa kilo moja wao hulipa zaidi ya dola mbili za kimarekani ambazo ni sawa na kati ya shilingi 3500 hadi 4000 bila kujali madaraja” alisema Kassia.

Akifafanua zaidi, alisema mtindo huo wa ununuaji umesababisha wakulima kuufurahia kwa kuwa hakuna utaratibu wala kujali madaraja ya ubora na kuikosesha serikali mapato.

 “Serikali ikizubaa na kufikiri kuwa tatizo hili litamalizwa na ushirika basi ijue kuwa yenyewe pia inaumia kwani na inapoteza mapato mengi,” alisema Kassia.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chutcu Sebastian Masika amewalalamikia askari wa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wafanyabiashara hao kwa uwapatia ulinzi na pia kuwavujishia siri za mikakati ya kuwadhibiti.

Na Moses Ng'wat Chunya