SIMU YAMTUPA GEREZANI MWAKA MMOJA




https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEisTf4z03UN6fFbsXX4v0ARIVVH2Jh8Tk6fu6yva2nY3mRm2AZBn5oLYyXc2D1dW4DC0lqm7o3a7282nla4PoMi_LT40eqr51p0MC7dVgLQZw4ZQlGGHa6o9aM3gR-wtOye3gw-k2IGWuIh/s1600/razr_phone.jpgMAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imemhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela, Fundi Mwashi Nassoro Mohamed (25), baada ya kukiri kosa la kutoa taarifa za uongo kwa kampuni za simu alipokuwa akisajili namba zake.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi, Hellen Riwa, baada ya mshtakiwa huyo kukiri kutenda kosa hilo Mei 27 mwaka huu.
Hakimu Riwa alisema kutokana na kosa la mshtakiwa kutuma ujumbe mfupi wa maandishi (sms) kwa viongozi wa serikali na kubainika alisajili kwa majina ya uongo, mahakama imemhumu kifungo cha mwaka mmoja au kulipa faini ya sh milioni 3.
Kabla ya hukumu hiyo, mshtakiwa aliiomba mahakama imhurumie kwa kuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa pumu na kwamba alishawahi kuugua ugonjwa wa figo kwa hiyo aliomba kifungo cha nje ili aweze kujikimu kimaisha.
Baada ya kukiri kosa hilo, Wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya, alimsomea maelezo ya awali na kuwaeleza maofisa wa polisi ngazi za juu makao makuu, walipata taarifa za kiitelejensia kwamba kuna mtu amesajili namba katika mitandao tofauti na anatuma sms kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Nchimbi na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP ), Saidi Mwema.
Alieleza baada ya upelelezi iligundulika kuwa namba 0687 521947, 0759 799956 na 0687521948 zilizosajiliwa kwa majina tofauti ya Fadhil Issah, Fadhil Issa na Godfrey Joseph ambazo zilikuwa za mshtakiwa.
Hata hivyo ujumbe wa simu uliotumwa kwa IGP Mwema na Dk. Nchimbi haukuainishwa mahakamani hapo.