TANGU ATUTOKE MWIGIZAJI MAARUFU WA BONGO MOVIE UMEPITA MWAKA MOJA


WAKATI Filamu ya marehemu Kanumba inayokwenda kwa jina la Power & Love ikitarajiwa kuzinduliwa keshokutwa (Jumapili) katika viwanja vya Leaders Kinondoni, jijini Dar es Salaam, yapo maswali mengi yameshaanza kujitokeza kwa wadau mbalimbali na mashabiki wa msanii huyo katika siku hiyo.


Filamu hiyo ambayo ndiyo ya mwisho kuicheza marehemu Kanumba na matukio yake yanaelezwa kuonesha namna gani alivyoweza kujitabiria kifo chake, itakwenda sambamba na kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu alipofariki dunia, kwani alifarika dunia tarehe na mwezi kama siku hiyo ya Jumapili.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, mdogo wa marehemu Kanumba, ambaye pia ni kiongozi wa ofisi yake ya ‘Kanumba The Great’ iliyopo Sinza, Seth Bosco, alisema katika uzinduzi huo zaidi ya waigizaji 10 kutoka Ghana wanatarajiwa kuwepo siku hiyo na hakutakuwapo na kiingilio.

Anasema mbali na waigizaji hao wa Ghana, pia rafiki wa marehemu, ambaye ni muigizaji maarufu barani Afrika, Mnigeria Ramsey Noah, pia anatarajiwa kuwapo.

“Ramsey tulimpigia simu na tukamtaarifu na akasema kuhusu uwepo wake siku hiyo atatujulisha kabla kama anakuja au la, kutokana na kuwa na majukumu mengi ya kikazi,” anasema Bosco.

Akizungumzia ratiba ya siku hiyo, alisema itaanzia nyumbani kwa marehemu, baada ya hapo wataelekea makaburini na baadaye Leaders kwa ajili ya uzinduzi huo.

Kabla ya kufanyika uzinduzi, Bosco anasema kutatanguliwa kwanza na ibada itakayoanza saa nne asubuhi na kwisha saa tano katika kanisa la Kimara, ambapo mashabiki wa filamu za Kanumba watatakiwa kufika asubuhi nyumbani kwa marehemu.

Anasema mara baada ya ibada hiyo, ndugu, jamaa, marafiki, waigizaji pamoja na mashabiki wake watakula chakula cha pamoja kisha kuelekea makaburini Kinondoni kabla ya kuingia viwanja vya Leaders.

Hata hivyo katika shughuli za uzinduzi bendi ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta ndiyo itahusika siku hiyo kwa upande wa burudani itakayokwenda sambamba na uuzwaji wa nakala za filamu hiyo papo hapo.

Katika filamu hiyo wameshirikishwa wasanii mbalimbali akiwamo Irene Paul, marehemu Sharo Milionea, Idrisa Kupa, Cathy Rupia na wengineo.

Marehemu Kanumba alifikwa na mauti Aprili 7, mwaka jana nyumbani kwake Sinza Vatican, huku kifo chake kikihusishwa na msanii wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’, ambaye kwa sasa yupo nje kwa dhamana baada ya kukaa maabusu kwa takriban miezi 10.