SITTI MTEMVU: "NIKA MIAKA 23, SINA MTOTO, WAANDISHI MNANIANDAMA" SAUTI NA VIDEO VIKO HAPA


Miss Tanzania 2014,Sitti Abbas Mtemvu akizungumza machache na waandishi wa habari. video ya alichokisema Miss Tanzania itawajia muda si mrefu.

 Mkurugenzi wa Lino International Agency ambao ni Waandaaji wa mashindano ya Urembo ya Miss Tanzania,Hashim Lundenga (kati) akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya sakata la umri halali wa Mrembo alietwaa taji hilo Mwaka huu, Sitti Abbas Mtemvu (kushoto),katika mkutano huo Lundenga alitolea ufafanuzi swala la umri wa Mrembo huyo kulingana na vilelezo alivyopewa na mrembo huyo wakati akijiunga na mashindano hayo
 Mkurugenzi wa Lino International Agency ambao ni Waandaaji wa mashindano ya Urembo ya Miss Tanzania,Hashim Lundenga akionyesha nakala ya cheti cha kuzaliwa cha Mrembo Sitti Mtemvu alicholetewa na wakazazi wake.
 Nakala halisi ya Cheti hicho inayoonyesha Mrembo huyo amezaliwa Mei 31,1991.
Miss Tanzania 2014, Sitti Mtemvu amevilaumu vyombo vya habari kwa kueneza habari za uongo kuhusiana umri na maisha yake binafsi. Mtemvu amesema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.

“Ukweli ni kwamba nina miaka 23 na cheti hicho hapo kinajielezea, mkitaka mnaweza kwenda hizo sehemu wanazotoa vyeti mkawauliza,” alisema Sitti. Mtemvu alisema cheti chake cha zamani cha kuzaliwa kilipotea akidai kuwa ni kutokana na maisha yake ya kusafiri mara kwa mara.

“Kwahiyo ilibidi pale walipohitaji cheti nilete kingine,” alijitetea.
 
“Sikutegemea hayo maswali leo kwahiyo sikuja nimejiandaa kihivyo,” alijibu mrembo huyo baada ya waandishi wa habari kumtaka awape ripoti yoyote ya polisi kuhusiana na kupotea kwa cheti chake cha mwanzo.
 
Cheti cha kuzaliwa alichonacho sasa kinaonesha kuwa kilitolewa September 9 mwaka huu.

Sitti alitumia pia fursa hiyo kukanusha tetesi kuwa ana mtoto. “Sina mtoto, na mkitaka tunaweza kwenda hospitali sababu naona kama mmekuwa mkiniandama kwa vitu ambavyo si vya kweli,” alisema.
 

Akijibu swali la kuonekana kwa passport yake inayoonesha kuwa alizaliwa mwaka 1989 na huku kwenye cheti alichoonesha kikionesha amezaliwa May 31, 1991, Sitti alisema:
 
Sitogusia hilo suala kwasababu mimi nilivyokuwa nakuja kuomba ‘Umiss Tanzania’ niliombwa cheti cha kuzaliwa sasa hivyo vitu vingine ni personal life, kwahiyo sidhani hata nyie kama kuna mtu atakuja anachukua passport yetu, ama driving licence ya kweli au feki na kuiweka kwenye mtandao kama ni kitu ambacho mngependelea.”
 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Lino International Agency Limited Hashim Lundenga alisema kuwa nafasi ipo wazi kwa wale wenye mashaka na umri na maisha ya Sitti kupeleka vielelezo halisi ambavyo watavifanyia kazi.


“Tukishapata proof tutazifanyia kazi vizuri sana na mwenye haki atapata. Sisi hatuwezi kumvua taji, vitahusika BASATA na wizara husika,” alisema Lundenga.
 
Kuhusu Sitti kudanganya kuwa na umri wa miaka 18 kama watu walivyodai ndivyo alivyosema, Lundega alidai kuwa hayo yamezushwa mtandaoni na kwenye shindano hilo hakuna aliyesema hivyo.
 
“Unaamini kwamba Sitti ana miaka 18?” alihoji Lundenga. “Sasa kama huamini yote yametoka kwenye vyombo vya habari. Sisi tunaamini cheti cha kuzaliwa, sasa kama kuna mtu ana doubt na cheti cha kuzaliwa aende RITA akafanye uchunguzi wake.”