MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es
Salaam, imemhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela, Fundi Mwashi Nassoro Mohamed
(25), baada ya kukiri kosa la kutoa taarifa za uongo kwa kampuni za simu
alipokuwa akisajili namba zake.
Hukumu
hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi, Hellen Riwa, baada ya mshtakiwa huyo
kukiri kutenda kosa hilo Mei 27 mwaka huu.
Hakimu
Riwa alisema kutokana na kosa la mshtakiwa kutuma ujumbe mfupi wa maandishi
(sms) kwa viongozi wa serikali na kubainika alisajili kwa majina ya uongo,
mahakama imemhumu kifungo cha mwaka mmoja au kulipa faini ya sh milioni 3.
Kabla
ya hukumu hiyo, mshtakiwa aliiomba mahakama imhurumie kwa kuwa anasumbuliwa na
ugonjwa wa pumu na kwamba alishawahi kuugua ugonjwa wa figo kwa hiyo aliomba
kifungo cha nje ili aweze kujikimu kimaisha.
Baada
ya kukiri kosa hilo, Wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya, alimsomea maelezo ya
awali na kuwaeleza maofisa wa polisi ngazi za juu makao makuu, walipata taarifa
za kiitelejensia kwamba kuna mtu amesajili namba katika mitandao tofauti na
anatuma sms kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Nchimbi na Mkuu wa Jeshi la Polisi
(IGP ), Saidi Mwema.
Alieleza
baada ya upelelezi iligundulika kuwa namba 0687 521947, 0759 799956 na
0687521948 zilizosajiliwa kwa majina tofauti ya Fadhil Issah, Fadhil Issa na
Godfrey Joseph ambazo zilikuwa za mshtakiwa.
Hata
hivyo ujumbe wa simu uliotumwa kwa IGP Mwema na Dk. Nchimbi haukuainishwa
mahakamani hapo.