WAALIMU WAJIPANGA KUPAMBANA



WAALIMU wilayani Ileje Mkoani Mbeya wamejipanga kukabiliana na aibu ya kufeli kwa wanafunzi kwa mwaka huu  baada ya matokeo ya darasa la saba na kidato cha nne mwaka jana kuto kuwa ya kulidhisha na kupoteza sifa ya miaka ya hapo nyuma ambapo ilikuwa ikiongoza kwa kutoa matokeo mazuri.

Waalimu hao wamekili waziwazi mbele ya kamati ya ukaguzi wa wilaya hiyo iliyo fanya ukaguzi wa kushtukiza katika shule za wilayani humo kufuatia kushuka kwa elimu.

Mmoja wa walimu hao kutoka shule ya msigi Chitete Galieti Kayinga alisema kuwa amekuwa akifundisha kwa muda mlefu na ufaulu kwa wanafunzi ulikuwa ni mkubwa na wenye sifa kwa Wilaya hiyo na Taifa kwa ujumla.

 Kayinga alisema kuwa hivi sasa elimu imeshuka kuanzia ngazi ya Wilaya, mkoa na taifa jambo ambalo alisema linapaswa kuangaliwa upya na viongozi wa Sekta ya elimu ili waweze kubaini chanzo cha kushuka kwa elimu nchini.

Aidha alisema kuwa jambo ambalo wamekusudia kulifanya katika wilaya hiyo ni walimu wote kujitoa kwa nguvu zote katika kufundisha wanafunzi wilayani humo ili waweze kurudisha sifa ambayo imeanza kupotea katika sekta ya elimu.

 Nae Afisa Elimu Sekondari wilayani Ileje, Jimmy Nkwamu alisema kuwa kutokana na ufaulu mbovu uliopo wilayani humo kwa wanafunzi wameamua kufanya ukaguzi wa kushtukiza ili kubaini tatizo lililopo.

 Nkwamu alisema kuwa wakaguzi hao wamebaini mapungufu na kuzungumza na walimu wa wilaya hiyo ili waweze kujitoa katika ufundishaji wa wanafunzi na kuirudisha hadhi ya wilaya hiyo.

 Aidha alisema kuwa tatizo linalozungumzwa na watu wengi kuwa walimu wanafanya mgomo wa chini chini kutokana na kutolipwa madai yao, suala hilo linaonekana kuwa siyo tatizo kwani walimu wenyewe katika mahojiano ya mmoja mmoja wamekuwa wakidai kuwa hakuna tatizo hilo.

 “Sisi tumejaribu kufanya mahojiano na walimu kwa kumuita mmoja mmoja lakini walimu hao wanasema kuwa hakuna tatizo la madai ya kutolipwa madai yao na wametuhakikishia kuwa wataendelea kufundisha vizuri kwa mwaka huu” alisema Nkwamu.

 Kwa upande wake Mkurugenzi wa Wilaya hiyo Sylvia Siriwa alisema kuwa mchakato walioufanya na wadau wa Elimu wilayani humo utasaidia kuhamasisha walimu, wazazi na wanafunzi kwa ujumla ili kuhakikisha wilaya hiyo inachukua tena nafasi ya pili au ya kwanza kitaifa.

 Siriwa alisema kuwa wilaya ya Ileje imejipanga vilivyo kutokana na matokeo mabovu kuanzia shule za msingi na sekandari jambo ambalo alikiri kuwa hiyo ni aibu kwa wilaya.