MBARALI: MTUMISHI ATIMULIWA KISA UBADHILIFU


BARAZA la madiwani wilayani Mbarali Mkoani Mbeya limefikia azimio la kumfukuza kazi Ferdinand  Manyele likimtuhumu kwa kuliingiza hasara halmashauri ya wilaya hiyo na wengine kupewa maonyo makali kwa kutumia vibaya ofisi.
 
Maazimio hayo yamefikiwa juzi katika mkutano wa baraza hilo la madiwani uliofanyika katika kumbi za halimashauri ya Mbarali ambalo lilikuwa likijadili tuhuma za ubadhilifu ulibainishwa na mkaguzi wa ndani wa serikali.

Baraza hilo la madiwani lilifikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa Mtunishi Manyele ameiingizia hasara kubwa halmashauri hiyo ya Mbarali kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa mbele ya madiwani hao na katibu wa baraza hilo, Brown Mwakibete ambaye ni diwani wa Mahongole.

Akisoma taarifa hiyo Mwakibete alisema kuwa mtumishi Manyele ameisababishia hasara halmashauri,  hivyo baraza linaagiza afukuzwe kazi na hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

“Mtumishi huyu ameisababishia hasala halmashauri, baraza linaagiza afukuzwekazi na hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yake,” alisema Mwakibete.

Aliwataja watumishi wengine wanaotakiwa kuchukuliwa kupewa maonyo makali ni pamoja na Eliya Mhecha, Dickson Maluchu  kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa Umma za mwaka 2003 kifungu cha V aya ya 56.

“Bakari Ramadhani baraza linaagiza hatua za kinidhamu zichuliwe na taarifa zimepelekwa Polisi wengine ni Mikidadi Mwazembe, Ponsiana Ngwando, Jordani Masweve wote hawa ni kwamujibu wa Ibara ya 47 kifungu cha pili (2),” alisema Mwakibete.

Aidha Mwakibete aliwataja wengine ambao watachukuliwa hatua za kisheria kuwa ni Engebelbert Maro, Mh. Diwani George Mbilla wa kata ya Ubaruku, na kuwa hawa nao pia wanatuhuma za utumiaji mbaya wa ofisi.

Baraza hilo lililokuwa limejawa na jazba za madiwani wa halmashauri ya Mbarali lilimalizika kwa shange baada ya madiwani hao kuona halmashauri inaondoa watu hao waliokuwa wananyonya pesa za wananchi kwa maslahi ya matumbo yao.

Kwa upandewake Maria Sokocho kutoka Ofisi ya katibu tawala wa mkoa wa Mbeya alisema kuwa madiwani wanawajibu wa kusimamia usomwaji wa mapato na matumizi katika vijiji vilivyopo katika kata zao ili kukabiliana na ubadilifu unao tokea katika vijiji.