RIWAYA NA ELIMTAA

RIWAYA: CHOKORAA
MTUNZI: George Iron Mosenya
CONT: 0655 727325

SEHEMU YA KUMI NA SITA

...
Akaingia hadi ndani. Akapigwa na mshtuko tena. Mlango wa chumba chake ulikuwa wazi.
Nani ameufungua!! Alijiuliza huku akiingia kwa umakini mkubwa.

Maajabu mengine makubwa kubebeka.
Picha ya mama Emma akiwa anatokwa jasho, kukoswakoswa na gari, mlango kwa wazi na sasa anashuhudia damu.
Alitokwa na yowe moja kubwa kisha akazirai.
Aliporejewa na fahamu alikuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Mauaji ya mwanasheria aliyeheshimika sana yalikuwa yanamuhusu.
Mwanaidi alijikuta akikata tama na kuamini sasa harakati zake zimefikia kikomo. Yote aliyoyahangaikia yameishia hapa alipofikia.
Hakuna wa kumpigania mtaani. Ni nani atakayemtetea.
Pingu zikaiunganisha mikono yake. Akapandishwa katika gari ya polisi.
Safari ya kuelekea rumande!!
Harakati za chokoraa zikaingia doa. Mkono wa dola ukamnasa.

*****

Emmanuel aliwasili hospitali saa moja baadaye akiwa amepita njia za uchochoro hapa na pale kuweza kuikwepa foleni ambayo haikuwa ya kutisha sana. Mwanzoni hakufahamu iwapo mkewe alikuwa amefikishwa hospitali, taarifa hiyo aliipata baada ya kufika nyumbani.
Aliambiwa msaidizi wa kazi za ndani.

Sasa alikuwa hospitali na kama alivyoambiwa awali kuwa mkewe yupo hoi. Kweli alikuwa hoi. Tena aliyepooza.
Emma alichanganywa na habari hii. Alijaribu kuuliza huku na kule hatimaye mwanaye wa kumzaa alimueleza juu ya ujio wa binti aliyeitwa Mwanaharusi.
“Sasa alimfanya nini hadi akawa hivi.” Emma aliuliza swali la kijinga wakati tayari alikuwa ameelezwa kuwa hakuna aliyeshuhudia tukio hili moja kwa moja. Bali wamemkuta mgonjwa katika hali mbaya zaidi ya hiyo aliyokuwa nayo wakati ule. Hakupata jibu.
Akahaha huku na huko. Bado hali haikuwa shwari.
Hospitali aliyolazwa mama Emma haikuwa mbali sana ana alipolazwa George asiyejitambua.
Huduma za madaktari ziliendelea kwa kasi ili kuokoa uhai huu.

Muda ulikwenda upesi sana. Msongo wa mawazo ukiwa umekijaza kichwa cha Emma. Siri na hatia kubwa aliyoandamana nayo ikaanza kumzidia. Alitamani kumshirikisha mtu lakini alikuwa amechelewa sana. Alikuwa ameua tayari!!.
Emma alikumbuka kuiangalia saa yake baadaye sana. Akagutuka ilikuwa saa tatu usiku!!
Akili ikafyatuka. Ikakimbia maili mia nyuma. Akakumbuka kitu!!
Sharti!!
Sharti alilopewa na mganga wa kienyeji. Muda ulikuwa unakaribia!!

Hakuna kitu kibaya kama kumtegemea mwanadamu katika jambo lolote lile na kumkabidhi maisha yako akuongoze. Kosa hili lilifanywa na mtu mzima huyu aliyehitimu chuo kikuu kasha kuwa mzembe katika kuisaka ajira hatimaye akajiingiza katika vitendo vya kishirikina.
Sasa ule utajiri wa kupewa na mwanadamu ukaanza kumtafuna.
Emma akaanza kulia. Waliomtazama walidhani anamlilia mkewe, lakini akilini alikuwa analia kilio cha majuto ambaye sasa anadeka kama mjukuu. Majuto ambaye hakutambuliwa wakati safari inaanza amejitokeza wakati huu mbaya.
Alikuwa na masaa matatu tu!!
Kuuondoa uhai wa mama George, kasha baada ya hapo atakuwa huru.
Atampatia wapi sasa mama George?? Hilo lilikuwa swali.

Emma akasimama wima kama mwendawazimu. Akaifikia gari yake. Akaingia ndani na kuiwasha kasha kwa mwendo wa kasi akaanza kuitafuta barabara ya Bagamoyo. Aweze kumuwahi mganga na kumwomba amuongezee muda. Hali ilikuwa tete.
Safari ilianza vyema sana. Lakini siku ya kufa nyani, miti yote huteleza. Na vita ya ardhini haiwezi.
Polisi wa usalama barabarani wenye njaa kali walimsimamisha.
Lahaula!! Alikuwa hajatembea na leseni wala kadi gari. Na kibaya zaidi alikuwa na kiasi kidogo sana cha pesa ambacho kisingewatosheleza askari wale kupeleka mboga nyumbani kwa ajili ya siku inayofuata.
Maneno matupu hayavunji mfupa!! Alibembeleza sana.
Walimwachia baada ya kuwaachia simu yake kama dhamana.
Dakika thelathini zikatokomea.

Sasa aliweza kuondoka.
Wakati Emma anaondoka. Kitanda kilichotulia kwa muda mrefu sasa kiliweza kuchezacheza kwa kiasi Fulani. Kasha kikacheza sana. Macho yakafunguka.
“George…..George yupo wapi.” Mwanamke aliyepooza upande mmoja aliuliza. Nesi wa zamu akatabasamu!! Mwanamke akaendelea kuuliza.
Hapo sasa akaitwa ndugu yake!! Swali lilikuwa lile lile.
“Namuhitaji hapa sasa hivi.” Aliamrisha.
Yule mtoto akatoweka na kwenda katika hospitali aliyokuwa amelazwa George.
Ilikuwa saa tano kamili usiku. George akashtuka kutoka katika usingizi wake wa kifo. Akaangaza huku na huku. Ile akili yake iliyofungwa na mwanadamu, ikawa huru.
Binadamu aliyeahidi kumuachia George akamuachia kweli baada ya muda wa masharti kupita.
Lile gogo pale kitandani. Likakaa kitako.
Hapakuwa na mtu chumbani. Na hakuna aliyetegemea gogo lile ipo siku litazinduka.
Aliyeagizwa akakumbana na maajabu haya.
George hakuwa chumbani!!
Nesi wa zamu na daktari aliyekabidhiwa jukumu la kulinda gogo lile kwa siri wakapigwa butwaa.
Daktari akajaribu kumpigia simu Emmanuel ili kumpa taarifa hii ya maajabu. Hakumpata hewani.
Hofu!!


*******

Mimi ni chokoraa!! Ni neno la kwanza alilokiri baada ya kuingia mtaani. Akili yake ilikuwa nyepesi sana. Tofauti na awali.
Mambo yote aliyoayaishi akiwa katika usingizi mzito lakini akinyanyaswa na sura ya Emmanuel ilimpatia picha ya yeye ni nani.
Emmanuel hakuwa mtu mzuri. Alikuwa ni shetani.

George akiwa ananuka madawa ya hospitali anaingia mtaani. Mtaa ambao alikuwa ni nia kubwa ya kuuokoa sasa anaingia akiwa anahitaji kuokolewa.
Frida, Isha, na Mwanaidi. Hili likawa wazo la kwanza juu ya wapi pa kuanzia aweze kupata hifadhi na kuusema ukweli wote anaoufahamu. Alihitaji kuusema ukweli huu ili amtie hatiani Emma aliyekuwa akimnyanyasa katika kijiji cha maajabu asichokijua.
Simulizi za akina Frida zilimbeba sana na kujua jinsi gani ya kuishi na watoto wa mitaani ili wasikuone kuwa u mgeni sana eneo lao. George hakutaka kujulikana kama yule George mtoto wa kitajiri. Hakutaka kuheshimika mtaani, alitaka kuishi alivyotakiwa kuishi.
Alitaka kuishi kichokoraa na afe akiwa chokoraa. Kama alivyozaliwa na kuamini kuwa alitupwa.
Usiku huu ukawa mwanzo wa safari ya George kuishi kichokoraa, ile hali ya kulala kitandani muda mrefu, kukosa chakula bora mtaani. Mabega yakapanda juu, macho yakabonyea ndani.
Watoto wa mtaani wakampachika jina jipya kabisa. Bonge!! Ikiwa ni utani wa waziwazi.
Bonge alikuwa mcheshi, asiyependa makuu, mkarimu. Na alionekana kama wa maajabu kwa jinsi alivyokuwa tayari kuwatetea wenzake hata mbele ya mgambo wa jiji. Alikuwa na majibu ambayo yaliburudisha masikio ya mgambo wa jiji na kushusha hasira zao.
Bonge alikuwa ni mtunzi wa hadithi na aliyajua maneno ya kuiteka hadhira yake.

Ni nadra sana kwa watoto wa mtaani kuheshimiana, lakini katika kempu hii ya Kariakoo mtaa wa gerezani heshima ilikuwepo. Kila mmoja kwa wakati wake alijikuta akimuheshimu mwenzake kutokana na nasaha za George ambaye alizoeleka kama Bonge.
Bonge aliyafurahia haya maisha.

Bonge naye ni mwanaume, tena mwenye hisia, japo moyo wake mkubwa uliwahi kumsumbua na kuingilia kipaji chake cha kucheza soka. Hii haikuwa na maana moyo ule ulipigwa ganzi katika suala la hisia.
Usiku huu palikuwa na baridi kali haswa. Handaki dogo walilokuwa wamejihifadhi watoto hawa wasiokuwa na kwao, lilipenyeza upepeo uliozidi kuwasulubisha. Bonge alikuwa kimya sana tofauti na kawaida yake ya kuwa msema mengi ili kuwaliwaza chokoraa wenzake.
Akiwa ametulia tuli. Alivamiwa na pepeo la maajabu, akahisi upweke na kujiona kuwa kuna kitu alikuwa anahitaji. Alihitaji joto.
Pepo la ngono likampanda bila kutarajia. Tena katika mzingira ya kustaajabisha.
“Kelvin…Kelv…” Bonge aliita kwa kunong’ona. Kelvin aliyekuwa anahangaika kuusaka usingizi aligeuka bila kusema lolote.
“Hivi Regina analala chimbo lile la ng’ambo bado.”
“Mh!! Analala palepale vipi kwani.”
“Aaah!! Basi tu..lala” alisema Bonge.
Kelvin hakujali akaendelea kuusaka usingizi.
Bonge akasimama kimya kimya. Akatoweka, hadi ng’ambo. Akamshtua Regina. Regina akaitikia wito.
Bonge akajielezea dhahiri kuwa amezidiwa. Regina akacheka sana kwa sauti ya chini. Hakuamini kama Bonge ana uhitaji huo.
“Namaanisha Regina kama una kiumbe nisaidie lakini usiambie mtu.” Alisihi Bonge.
“Nisubiri pale ‘chemba’ Bonge la bwana.” Aliongeza nakshi katika lile jina. Wote wakacheka.
“Regy…..asiwe ananijua…” alitoa maelekezo Bonge.

Kisha akachukua nafasi katika chemba aliyoelekezwa. Baada ya muda akasikia hatua zikijongea eneo lile.
Mapigo ya moyo ya Bonge yakaongezeka huku tama nayo ikichukua nafasi.

*******


*****

Mcha Mungu kamwe hawezi kumficha mwovu.
Licha ya kukosa nafasi ya kuzungumza na George baada ya kuwa amerejewa na fahamu. Hakusita kuuelezea umma juu ya kilichojiri, hasahasa polisi ambao walichukulia hili jambo uzito.
Emma alitoweka kwa siku tatu. Siku zisizokuwa na mafanikio.
Alirejea nyumbani kisirisiri ili kuchukua pesa katika amana zake ili aweze kumpatia mganga waendelee na zoezi la kumsaka George ambaye alikuwa ameachwa huru.
Siku aliyorejea kwake ikawa siku ya mwisho kuwa huru mtaani.
Mama mcha Mungu. Akauweka uongo kando akayatua mapenzi ya kupendana na mfuasi wa shetani. Akatoa taarifa polisi.
Bwana Emma akakamatwa.
Ikiwa ni mara yake ya kwanza kulala rumande tangu azaliwe.

Maswali mawili matatu ya mitego. Akanasa.
Makofi mawili matatu. Akausema ukweli.
Kipigo kitakatifu akakiri kuwa alimuua Mwanasheria Kindo.

Salamu za kushangaza tena za wakati muafaka zikawafikia wale wanaoonewa gerezani. Mwanaidi, Frida na Isha. Wote wakaachiwa huru. Aliyetakiwa amepetikana. Chokoraa wasiokuwa na hatia wakarejea mtaani. Bado hakuwepo wa kuwapokea, ni mtaa uleule usiobadilika ukawasabahi.
Kila mmoja alitolewa kwa wakati wake.
Mwanaidi kivyake lakini Frida na Isha walioshtakiwa kwa kosa moja waliachiwa pamoja.
Ilikuwa majira ya mchana. Wakaingia tena mtaani wakiwa hoi. Lakini huru.
Mtaa mmoja baada ya mwingine, hatimaye mguu wao wa mwisho unaishia mtaa wa Kariakoo gerezani.
Ni hapa waliamini wanaweza kujihifadhi na wenzao.
Usingizi wa mang’amung’amu unakatizwa na amri kutoka kwa dada mkubwa wa kempu.
Frida akiwa amesinzia, Isha anaamshwa na kuamriwa afunge tela amfuate dada mkubwa.
Safari yao inaishia katika chemba yenye giza.

Anasukumiwa ndani, anapokelewa na mikono kakamavu ya kiume. Hakuna mazungumzo
Anajua nini kinachoendelea binti huyu analia kwa kusihi, “Kondomu…kondomu….” Kinga pekee ndiyo msaada anaoamini anaweza kufanyiwa lakini sio chokoraa kusamehewa katika kubakwa. Ni kawaida yao kubakwa. Wanaonewa.
Mwanaume anasita kwa muda anafanya tafakari kilio kile cha mwanamke. Tamaa inazidi nguvu maamuzi. Anamkumbatia yule msichana aliyekondeana.
“Bonge kuna UKIMWI…kuna kisonono, kuna fangasi…Bonge…Bonge!! Shauri zako.” Sauti ilimwambia katika nafsi yake. Akatamani kuacha lakini alikuwa amtamanika tayari!! Angefanya nini.
Akaitawanya kanga ya yule binti. Akaanguka naye chini. Badala ya kutua chini wakatua katika kitu kingine. Kikaunguruma.
Wakatulia. Bonge suruali magotini, binti kanga pembeni.
Kikaunguruma tena.
Hapa sasa Bonge akawa mwanariadha mzuri, huku Isha akimfuatia kwa kasi.
Walienda pande mbili tofauti.
Dada mkubwa Regina naye alishtushwa na hali hii. Chokoraa hana ngojangoja. Naye akatimua mbio.
Walifurahisha kuwatazama.

****Ni kitu gani kimekatisha dhambi hii ya CHOKORAA…….

****BONGE, ISHA NA MWANAIDI NA FRIDA je wataonana tena!!

***LIKES NA SHARES PAGE HII IWAFIKIE WENGI ZAIDI NA ZAIDI.
ITAENDELEA………
See More