CCM Yajipanga Kushinda 2020

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Seif Ali Iddi amemhakikishia Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Dk Abdalla Juma Abdalla ushirikiano wa dhati kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake na kuona CCM inashinda katika Uchaguzi Mkuu ujao wa 2020.
Balozi Iddi ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda alisema hayo wakati akimkaribisha katika Mkoa wa Kaskazini Unguja Naibu Katibu Mkuu, Dk Abdalla kutokana na uteuzi wake mpya wa kushika wadhifa huo kuongoza CCM Zanzibar.
Alisema CCM imekabidhiwa jukumu kubwa la kupewa dhamana ya kushika dola na wananchi baada ya kuipa ridhaa kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa marudio ya mwaka 2016 ambao utekelezaji wa Ilani ya CCM ni muhimu ili kutoa nafasi ya kupewa ridhaa nyingine. Alisema Mkoa wa Kaskazini Unguja unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuwepo kwa mikakati zaidi ambayo utaifanya CCM kupambana na upinzani.
“Tunakukaribisha katika Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo tunaahidi kukupa ushirikiano wa dhati ambao utahakikisha Chama Cha Mapinduzi kinaimarika katika mkoa wa kaskazini Unguja ikiwemo kuingiza wanachama wengi zaidi,” alisema.
Akizungumza katika mkutano huo, Dk Abdalla maarufu Mabodi, alisema huu ni wakati wa kufanya kazi, hivyo viongozi wanatakiwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi pamoja na ahadi zao kwa wapiga kura. Alisema Ilani ya Uchaguzi ndiyo makubaliano ya wananchi na chama ambapo kwa viongozi wanatakiwa kuyasimamia kikamilifu na kuona chama kinapiga hatua kubwa ya kuelekea katika ushindi.
Aliwaonya baadhi ya viongozi ambao wameacha kusimamia na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi na kwa sasa wapo katika harakati za kupanga safu ya uongozi. “Huu si wakati wa kupanga safu za uongozi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2020… tunakabiliwa na jukumu kubwa la kutekeleza ilani ya uchaguzi ya 2015-2020 ambayo ndiyo makubaliano kati ya chama na wapiga kura,” alisema.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Haji Juma Haji aliahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa Naibu Katibu Mkuu mpya huku akiweka bayana CCM kuchukua majimbo yote ya mkoa huo. Alisema wamejipanga vizuri ikiwemo kuingiza wanachama wapya kupitia jumuiya mbalimbali za CCM katika hatua ya kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
“Tumejipanga vizuri sana kwa upande wa mkoa wa kaskazini Unguja na tunaahidi kuyachukua majimbo yote ambayo baadhi yamechukuliwa na upinzani CUF,” alisema. Majimbo mawili katika Mkoa wa Kaskazini Unguja yamechukuliwa na CUF ambayo ni Nungwi na Bumbwini.

from Blogger http://ift.tt/2pxEx3g
via IFTTT




from WordPress http://ift.tt/2pdF6CG
via IFTTT