Wagoma kuandikishwa kata mpya Wanging'ombe


WANANCHI wa kijiji cha Itengelo kata ya Saja wamegoma kuendelea kuandikishwa katika daftari la kudumu la mpigakura kwa mfumo wa kielektroniki (BVR) kufuatia uongozi wa kijiji hicho kuwahamishia katika kata mpya ya Uhenga badala ya kata ya zamani Saja, halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe mkoani hapa.

Mgomo huo umetokea juzi katika kata hiyo ambapo wananchi hao walitakiwa kujiandikisha katika kata ya Saja na kutakiwa kuhamishiwa katika kata ya Uhenga ambako serikali ya kijiji hicho ilitaka wahamie huko.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wa kijiji cha Uhenga walisema wanapinga kupelekwa katika kata ya Uhenga badala yake wabaki katika kata ya Saja kwa kuwa kata ya Uhenga iko mbali na imewapelekea kushindwa kupata huduma ikilinganishwa na Saja walikozoea.


Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Gaston Mlimbila alilamikia kitendo cha wananchi kushindwa kushirikishwa wakati wa uanzishwaji wa kata mpya lakini katika hali ya kushangaza wananchi hao hawakushirikishwa jambo ambalo wao hawako tayari kujiandikisha kwenye kata ambayo wao hawaitambui.

“Tunagoma kujiandikisha katika daftrari hili, kwa kuwa upande wa akina mama tumezoea kwenda hapa katika kliniki ya Saja sasa wakitupeleka huko Uhenga ina maana itabidi tutembee umbali wa kilomita 12 kufuata huduma za afya,  hili hatukubali,” alisema Aziza Mbwilo mkazi wa kijiji hicho.

Diwani wa Kata ya Saja Andrew Mangula pamoja na kuwashi wananchikwenda kujiandikisha juhudi zake ziligonga mwamba baada ya wananchi kushikilia msimamo wa kugomea kwenda kujiandikisha kwa madai kuwa hawataki kujihalalisha kuwa wakazi wa kata ya Uhenga.

“Ombi lenu la kutaka kubaki katika kata mama ya Saja litashughulikiwa lakini mchakato wake hauwezi kwenda haraka kama mnavyotaka, mchakato ni mrefu mno maana hata sisi tutaanza nalo lakini watakao kuja kuendelea na mchakato huu hadi ukamilike ni viongozi mtakaowachagua mwaka huu,” alisema Mangula..

Aliwataka wanakijiji hao kuanza mchakato wake huo sasa, lakini suala hilo linabidi lipitie hatua mbalimbali hadi kukamilika, ikiwa ni pamoja na kujadiliwa na Baraza la Maendeleo la Kata (BMK), Kikao cha Baraza la Madiwani na hatimaye kwenda kwenye kikao cha ushauri cha maendeleo ya wilaya (DCC) na kile cha mkoa (RCC) na kasha kwenda Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa ajili ya kupitishwa..

Hata hivyo diwani Mangula alimtupia lawama mwenyekiti wa zamani kijiji hicho Henry Ngajule kwa kushindwa kutoa mrejesho kwa wananchi wake baada ya maazimio yaliyokuwa yakijadiliwa kwenye BMK.


Alipotafutwa kutolea ufafanuzi juu ya uamuzi wa wananchi wa kata ya Uhenga kugomea kujiandikisha, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe Emmanuel Kilundo alisema kwa njia ya simu kwamba atalitolea ufafanuzi suala hilo baada ya kupata taarifa juu ya suala hilo.